WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Yahya Ahmed Okeish na kujadiliana masuala mbalimbali yakiwemo ya kilimo, uvuvi na uwekezaji.
Akizungumza na balozi huyo leo (Jumatano, Desemba 13, 2023) ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema anatambua matunda ya uhusiano wa muda mrefu ambayo Tanzania imeyapata kutoka Saudi Arabia ikiwemo misaada kwenye sekta za afya, elimu na maji.
“Natambua dhamira ya Saudi Arabia kuja kuwekeza kwenye kilimo, wakiwa tayari tutawapokea na natumaini watatumia vizuri fursa hiyo kuendeleza kilimo. Lakini pia tunazo fursa za uwekezaji za uvuvi kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Nitumie fursa hii kukaribisha kampuni za Saudi Arabia zije kuwekeza kwenye uvuvi wa bahari kuu kwani huko kuna samaki aina ya tuna.”
Waziri Mkuu ameishukuru nchi hiyo kwa kukubali kununua nyama kutoka Tanzania na akatumia fursa hiyo kuwaomba waongeze wigo wa kununua nyama zaidi na kuwahakikishia kwamba Tanzania itaendelea kuwapatia nyama yenye viwango bora.
Aliipongeza Serikali ya nchi hiyo kwa uamuzi wake wa kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Tanzania kwani zitasaidia kuimarisha utalii na watu wanaokwenda hijja. “Ninayo taarifa kwamba hivi karibuni, Shirika lenu la ndege litaanza pia safari za moja kwa moja kutoka Saudi Arabia hadi Zanzibar. Hii si tu kwamba itasaidia kuongeza idadi ya watalii bali pia itawawezesha watu wanaoenda umra na hijja,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa alitumia fursa hiyo kumpongeza Mfalme wa nchi hiyo, King Salman Bin Abdulaziz Al Saud na Waziri Mkuu wake, mwanamfalme Mohammed Bin Salman Bin Abdulaziz Al Saud kwa ushindi ambao nchi yao imeupata ili kuwa mwenyeji wa maonesho ya kimataifa duniani ya Expo 2030.
Maonesho hayo makubwa duniani, yanatarajiwa kufanyika jijini Riyadh kuanzia Oktoba, 2030 hadi Machi 2031. Saudi Arabia ilipata ushindi wa kura 119. Majiji mengine yaliyokuwa yakiwania nafasi hiyo ni Busan (Jamhuri ya Korea) na Roma (Italia).
Mapema, Balozi Okeish alitoa pole kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maafa makubwa yaliyotokea Katesh, wilayani Hanang lakini akaipongeza kwa jitihada ilizofanya kuokoa maisha ya walionusurika na kurejesha huduma kwa wananchi hao.
Alimweleza Waziri Mkuu kwamba amekutana na wafanyabiashara wengi wa Saudi Arabia ambao kwanza wamekubali kuja kutembelea Tanzania lakini pia wako tayari kuunda Baraza la Wafanyabiashara baina ya Tanzania na Saudi Arabia.