Makamu wa rais ahimiza matumizi ya hatifungani kuharakisha maendeleo

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameielekeza TAMISEMI na Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhamasisha matumizi ya dirisha la Hatifungani ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 Ofisi ya hazina ndiyo msimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma nchini na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI ndiyo msimamizi wa Halmashauri zote zilizopo nchini Tanzania.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo wakati wa Uzinduzi wa Uuzaji wa Hatifungani kwaajili ya Fedha za Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Maji, Tanga uliyofanyika katika Ukumbi wa Regal Naivera Jijini Tanga. 

Mpango amesema Hatifungani iliyozinduliwa mkoani Tanga inapaswa kuwa chachu na motisha kwa Halmashauri na taasisi nyingine kutumia njia hiyo kupata fedha za miradi ya maendeleo na kutoa nafasi kwa Serikali kujikita kwenye maeneo mengine ya kipaumbele ambako hakuna uwezeshaji wa aina hiyo.

 Aidha Makamu wa Rais ameitaka Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga, kusimamia vizuri matumizi ya fedha zitakazopatikana kupitia Hatifungani iliyozinduliwa na mapato mengine yatakayokusanywa baada ya kukamilisha mradi huo. 

Amesema nidhamu ya fedha na usimamizi thabiti ndiyo utakaowawezesha kurejesha kwa wakati fedha za wawekezaji wa Hatifungani hiyo na Serikali haitavumilia uzembe wa aina yoyote utakaoonekana kukwamisha jitihada hizo.

Jumla ya shilingi bilioni 53.12 zinatarajiwa kuwekezwa katika Hatifungani ya Kijani ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu ya maji.

Share: