Zanzibar kununua sukari kutoka mahonda

Matumizi ya Sukari huongezeka zaidi katika Mwezi wa Ramadhan na unakaribia hivyo ni vyema tukazalisha kwa wingi na tukategemea Sukari ya kwetu kuliko kusubiri kutoka nje ya nchi

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itanunua Sukari inayozalishwa katika Kiwanda cha Sukari Mahonda ili kuwaondoshea usumbufu Wananchi. Akizungumza na Uongozi wa Kiwanda hicho mara baada ya kufanya ukaguzi wa uzalishaji wa bidhaa hiyo Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaaban amesema bei ya Sukari Imepanda hivyo kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) imeamua kuchukuwa hatua hiyo ili kurahisha upatakinaji hasa katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambacho bidhaa hiyo inatumika kwa wingi.

"Matumizi ya Sukari huongezeka zaidi katika Mwezi wa Ramadhan na unakaribia hivyo ni vyema tukazalisha kwa wingi na tukategemea Sukari ya kwetu kuliko kusubiri kutoka nje ya nchi" alisisitiza Waziri Shaaban. Amesema Serikali itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano katika Kiwanda hicho ili kuhakikisha uzalishaji unaongezeaka na kuleta tija kwa Wananchi wa Zanzibar.

Aidha amefahamisha kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Sukari inayozalishwa haitoki nje ya Zanzibar ili kuondosha malalamiko ya Wananchi yanayotokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo."Sukari iliyokuwepo ndani ibaki hapa hapa kwetu kwani kuna baadhi ya Watu wanatoka nje ya Zanzibar kufuata Sukari huku na kusababisha Wananchi kukosa Sukari hiyo "alibainisha Waziri huyo.

Nae Meneja Rasilimali Watu kutoka Kiwanda Cha Sukari Mahonda Bashiru Wazir Muhamed amesema wanatarajia kuzalisha tani elfu tano, iwapo hakutakua na mvua ambayo itaathiri uzalishaji.Hata hivyo amefahamisha kuwa uzalishaji huo umeanza February 9 mwaka huu kutokana na hali ya kuwepo kwa mvua jambo ambalo lililopekea kuchelewa kuanza uzalishaji huo.

Share: