Serikali imeendelea kuboresha ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa luku kwa nyumba zenye mita zaidi ya moja kwa kuhakikisha inalipiwa mita moja pekee
Serikali imewataka wamiliki wote wa majengo wenye changamoto za ulipaji kodi ya majengo kupitia ununuzi wa umeme ikiwa ni pamoja na uwepo wa mita zaidi ya moja katika jengo, wafike katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyokaribu nao kwa ajili ya kufanya maboresho ya taarifa zao.
Rai hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Nyamagana, Mhe. Stanslaus Shing'oma Mabula, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kutenganisha malipo ya majengo kwa nyumba yenye zaidi ya mita moja ya umeme.
“Serikali imeendelea kuboresha ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa luku kwa nyumba zenye mita zaidi ya moja kwa kuhakikisha inalipiwa mita moja pekee”, alieleza Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema kuwa inapobainika majengo mawili au zaidi yanatumia mita moja, Serikali imekuwa ikifanya maboresho ya ukusanyaji wa mapato kwa kutoza kiasi kinachopaswa kulipwa kwa kila jengo kwa mita iliyopo, lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha msingi wa utozaji wa kodi ya majengo unazingatiwa.