Waziri mkuu afungua wiki ya huduma ya fedha kitaifa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Fedha iimarishe mifumo ya kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha ili baadhi ya watoa huduma wasio waadilifu wasitumie changamoto ya uelewa mdogo wa masuala ya fedha kwa baadhi ya wananchi na kuwadhulumu.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Wizara ya Fedha iendelee kushirikiana na watoa huduma za fedha kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo muhimu yakiwemo ya usimamizi wa fedha binafsi, kuweka akiba, mikopo, uwekezaji kupitia hatifungani na hisa, bima, mpango wa kujiandaa na maisha ya uzeeni pamoja na kodi.

“Wizara ya Fedha iandae mpango maalumu wa kutoa hamasa kwa Watanzania ili wajenge utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha, pia elimu iendelee kutolewa kuhusu wajibu wa kila mmoja kudai na kutoa risiti kwa malipo yanayofanyika. “

Ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Novemba 22, 2023) alipofungua Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa, jijini Arusha, ambapo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watoa huduma za kifedha wapunguze gharama za upatikanaji wa huduma za fedha zikiwemo riba na ada ili wananchi wengi watumie huduma za fedha zilizo rasmi.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameisisitiza Wizara ya Fedha iendelee kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Programu ya kutoa elimu ya fedha kwa umma na kuhakikisha kuwa elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.

Waziri Mkuu amesema Wizara ya Fedha inatakiwa iandae mpango maalumu wa kutoa hamasa kwa Watanzania ili wajenge utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha pamoja na kuratibu gharama za huduma za fedha. “Pia, elimu iendelee kutolewa kuhusu wajibu wa kila mmoja kudai na kutoa risiti kwa malipo yanayofanyika.“

Waziri Mkuu amesema watoa huduma za kifedha hawana budi kujenga uelewa wa kutosha kwa wananchi kabla ya kufunga nao mikataba, pamoja na kuwafafanulia taratibu na masharti yao kabla hawajatoa kwao huduma hizo za fedha. Pia amewataka watoa huduma hao waweke mkakati mahususi wa kuongeza matumizi huduma kwa njia ya kidijitali pamoja na kuzisogeza hadi maeneo ya pembezoni na vijijini ili wananchi walio wengi wanufaike.

Share: