Waziri mchengerwa: 'samia bond' kuwasaidia wakandarasi wazawa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa ameelekeza TARURA kuanzisha mchakato wa upatikanaji wa hati fungani ya miundombinu ya Barabara (TARURA Infrastructure Bond) ambayo itaitwa ‘Samia Bond’ kwa kushirikiana na taasisi za kifedha nchini.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo Januari 24, 2024 kwenye kikao kazi chake na Menejimenti ya TARURA, Makatibu Tawala Wasaidizi (Miundombinu), Makandarasi Wazawa,Wataalamu Washauri na Taasisi za Kibenki kilichofanyika leo kwenye ukumbi wa kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Mwl.Nyerere (JNICC )jijini Dar es Salaam.

Waziri Mchengerwa amesema lengo la kuanzishwa kwa hati fungani hiyo ni kuwasaidia Makandarasi Wazawa kukabiliana na changamoto za kifedha wanazokumbana nazo na kuwawezesha kupata kazi za miradi mikubwa na waweze kuikamilisha kwa Ufanisi.

Hata hivyo amesema ndoto yake ni kuwatengeneza Wakandarasi wazawa mabilionea ambao watafanya kazi bila kushikwa mkono na kuishi ndoto ya kumsaidia Rais Dkt. Samia.

Kikao kazi hicho kwa upande wa TAMISEMI Kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa OR TAMISEMI Mhe.Deo Ndejembi,Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Miundombinu Mhandisi Rogatius Mativila,Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff, wawakilishi wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya TAMISEMI pamoja na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini.

Share: