Watumishi wizara ya fedha watakiwa kuendelea kuzingatia sheria

maagizo yaliyotolewa na yatakayoendelea kutolewa na viongozi yanafanyiwa kazi kwa ufanisi kwa ustawi wa Taifa kwa ujumla.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amewataka watumishi wa wizara hiyo kuendelea kuzingatia misingi ya utawala bora na sheria katika utekelezaji wa majukumu yao ili kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuleta mageuzi na mabadiliko ya kiuchumi nchini.

Dkt. Mwamba alitoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa ni muhimu watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano kati ya idara na vitengo ndani ya wizara na taasisi kwa kuboresha mifumo ya usimamizi wa fedha na mali za umma pamoja na kufanya ufuatiliaji na kaguzi za mara kwa mara ili kujiridhisha na ubora wa miradi na thamani ya fedha zinazotumika.


‘‘Tutekeleze majukumu yetu kwa weledi, ubunifu na uadilifu, ni muhimu kuandaa programu za mafunzo ya masuala ya kitaaluma, utaalamu, maadili na umahiri mahali pa kazi. Programu hizo zizingatie mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika mifumo ya usimamizi wa uchumi, fedha, mipango, mazingira na utawala bora’’, alisema Dkt. Mwamba.

Aidha, Dkt. Mwamba alisema kuwa anatambua utendaji kazi na kuthamini mchango wa kila mtumishi wa wizara na taasisi zake katika utekelezaji wa mipango ya Serikali na kusisitiza kuendelea kuwajengea uwezo kupitia mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ubora unaostahili.

Akizungumzia Baraza la Wafanyakazi, Dkt. Mwamba alisema kuwa Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu la majadiliano mahali pa kazi, ambalo limeundwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo ili kutoa fursa ya majadiliano ya masuala ya ajira na mazingira ya kazi kati ya mwajiri na waajiriwa.

‘‘Ni lazima tutambue kuwa mikutano kama hii inatupa fursa ya kuzungumza na kujadili masuala ya msingi ya utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau wetu. Inatupasa kutambua kuwa Wizara ya Fedha ni taasisi muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, hivyo hii ni fursa ya kujadiliana masuala mbalimbali ili kuboresha utendaji wetu wa kazi’’, alifafanua Dkt. Mwamba.

Alisisitiza wajumbe kujadili kwa uwazi na kufanyia kazi masuala yote yatakayoibuliwa na kuwa ofisi yake ipo wazi kupokea na kujadili hoja zote za kiutumishi, kiutawala na kiutendaji ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi na huduma kwa wadau.


Mkutano huo wa siku mbili umekutanisha wajumbe kutoka Wizara ya Fedha pamoja na taasisi zilizo chini yake kwa ajili ya kusikiliza mawasilisho mbalimbali, kujadili kwa uwazi pamoja na kufanyia kazi masuala yote muhimu yatakayo ibuliwa katika mada hizo na kuboresha utendaji kazi kwa maslahi mapana ya Taifa. 

Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo, alisema kuwa kikao hicho kinafanyika kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini sura namba 336 kwa lengo la kuongeza ushirikishwaji wa watumishi katika masuala mbalimbali ya Wizara. 


‘‘Niwapongeze kwa maandalizi mazuri na niwasihi wajumbe kujadili masuala ya msingi kwa maendeleo ya Wizara na Taifa kwa ujumla, kusikiliza na kuchangia mada mbalimbali zitakazowasilishwa na kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kujadili maendeleo ya Wizara’’, alisisitiza Bi. Omolo.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Fedha Bi. Scholastica Okudo, alisema kuwa watumishi wa Wizara ya Fedha wamejipanga kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi kuhakikisha kuwa maagizo yaliyotolewa na yatakayoendelea kutolewa na viongozi yanafanyiwa kazi kwa ufanisi kwa ustawi wa Taifa kwa ujumla.

Aidha alisema kuwa watumishi wamejipanga kuhakikisha kuwa masuala yote ya kiutendaji yanafanyika kwa kufuata Sheria kanuni na taratibu na pia kuhakikisha kuwa wanazuia mianya ya rushwa inayoweza kujitokeza na Imani yao ni kuwa mifumo iliyoweka na Serikali inasaidia katika kuzuia mianya ya rushwa.


Share: