Watanzania wapewe kipaumbele  mradi wa eacop-dkt. biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watendaji katika kampuni inayotekeleza Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kuhakikisha kuwa, Watanzania wanapewa kipaumbele katika hatua zote za utekelezaji wa mradi ikiwemo ajira na utoaji huduma kama vile ulinzi, chakula, usafiri, bidhaa za ujenzi, huduma za mawasiliano na huduma nyinginezo ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015.

Dkt. Biteko amesema hayo mara baada ya kufanya ziara katika kata ya Chongoleani jijini Tanga na kujionea kazi mbalimbali za ujenzi wa miundombinu zikiendelea katika eneo hilo ambalo mafuta kutoka nchini Uganda yatakuwa yakipokelewa na kuhifadhiwa kabla ya kusafirishwa. Katika ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Bendera na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Kuhusu ujuzi unaotolewa na kampuni ya EACOP kwa watanzania wakiwemo kutoka vijiji vinavyozunguka mradi, Dkt. Biteko ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha inatoa ujuzi ambao ni endelevu utakaowawezesha kuendelea na kazi hata pale mradi utakapokamilika akitolea mfano kuwawezesha kupata mashine za uchomeleaji ambapo ametaka Halmashauri zishirikiane na kampuni ili kutekeleza suala hilo.

Akizungumzia utekelezaji mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi litakalokuwa na urefu wa kilomita 1,443 amesema kuwa, unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 32 na mabomba yatakayopitisha mafuta yanaendelea kuingia nchini kwa ajili ya kuwekewa mifumo ya upashaji joto na plastiki itakayozuia upotevu wa joto kwenye mabomba hayo katika kiwanda kilichopo Sojo wilayani Nzega.




Share: