Wafanyakazi wa mgodi wa dhahabu cata mining wameanza mgomo wa kutofanya kazi na kuamua kulala katika ofisi za mgodi huo

Wafanyakazi wa mgodi wa Dhahabu CATA MINING uilioko Kijiji Katalyo Wilayani Butiama Mkoani Mara, wameanza mgomo wa kutofanya kazi na kuamua kulala katika ofisi za mgodi huo, wakishinikiza uongozi wa Mgodi kuwalipa malimbikizo ya mishahara yao.

Mbali na Mishahara wafanyakazi hao wanadai michango yao katika mfuko wa hifadhi ya Jamii NSSF kutowasilishwa na mwajiri wao, licha ya michango hiyo kukatwa kwenye mishahara yao zaidi ya miaka saba sasa.

Wafanyakazi hao zaidi ya 200, wanadai mishahara yao ya miezi miwili, Novemba na Desemba 2023, ambapo toka jana wameanza mgomo wa kutofanya kazi wakishinikiza kulipwa kwa madai hayo.

Hii siyo mara ya kwanza kwa wafanyakazi wa Mgodi huo, kuingia mgogoro na mwajiri wao, ambapo mwaka jana 2023, walianzisha mgomo kama huu kushinikiza walipwe madeni ya mishahara ya miezi mitatu Julai, Agosti, na Mwezi Septemba.

Mgogoro huo ambao ulifika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, ambapo mwajiri alikiri kudaiwa na kuhaidi kulipa jambo ambalo alilitekeleza kwa kuwalipa wafanyakazi wote, na sasa hali hiyo imejirudia tena.

“ Hii ni mara ya Pili, tumeamua sasa kuanzisha mgomo wa kutofanya kazi mpaka pale tulipwe mishahara na michango ya NSSF, tumeamua pia kulala na kushinda hapa mgodini, mpaka pale tutakapolipwa madeni yote,” amesema mmoja wa fanyakazi.

“Uongozi wa Mgodi huu umekuwa kero kubwa sana, kila siku tukiulizia mishahara yetu wanatupiga chenga tu, tumeamua pia kuandika barua kwa waziri wa Kazi, na Waziri wa Madini, tukiwaomba watusaidie hili jambo, tunamwomba Mama yetu Rais atusaidie hili jambo,” alisema mfanyakazi mwingine.

Picha mbalimbali za video na mnato, zimepigwa zikionyesha wafanyakazi hao wakiwa wamelala usiku mgodini hapo, ambapo walieleza kuwa hawatajali watalala siku ngapi mpaka pale watakapolipwa madeni yao.

“ Kwa sasa watoto wetu wanataka kwenda shule, hatuna hata pesa za kuwapeleka shule, Tunaomba msaada kwa viongozi wa serikali watusaidie tuweze kupata haki yetu,”

Tumeutafuta uongozi wa juu wa mgodi huo kuelezea madai hayo akiwemo Mkuu wa Utumishi mgodini hapo (HR) Richard Bendera lakini hatukuwemo kufanikiwa kuwapata, ambapo simu zao ziliita mara kadhaa bila ya upokelewa.

Share: