Ukarabati wa piramidi ya misri wazua mjadala

Video inayoonyesha kazi ya ukarabati katika piramidi ya Menkaure ya Misri huko Giza imezua ukosoaji kwenye mitandao ya kijamii, huku mtaalamu mmoja akikemea "upuuzi" wake.

Mostafa Waziri, mkuu wa Baraza Kuu la Mambo ya Kale la Misri, ametofautiana na wakosoaji hao na kuuita "mradi wa karne."

Katika video iliyotumwa kwenye Facebook siku ya Ijumaa, Waziri alionyesha wafanyakazi wakiweka vitalu vya granite kwenye msingi wa piramidi, ambayo iko kando ya sphinx na piramidi kubwa zaidi za Khafre na Cheops huko Giza, Ukarabati huo unalenga kurejesha mtindo wa awali wa muundo kwa kujenga upya safu ya granite.

Kazi hiyo inatarajiwa kudumu kwa miaka mitatu na itakuwa "zawadi ya Misri kwa ulimwengu katika karne ya 21", alisema Waziri, ambaye anaongoza misheni ya Misri na Japan inayosimamia mradi huo.

Lakini chini ya video hiyo, watu kadhaa waliokasirika waliacha maoni ya kukosoa kazi hiyo, wengi wakisema inabadilisha uasili wake.

Suala la uhifadhi wa urithi nchini Misri ambalo linapata asilimia 10 ya pato lake la ndani kutokana na utalii, mara nyingi ni mada ya mjadala mkali.

Uharibifu wa hivi majuzi wa maeneo yote ya eneo la kihistoria la Cairo ulisababisha uhamasishaji wenye nguvu na mashirika ya kiraia, ambayo kwa kiasi kikubwa yamepigwa marufuku kufanya shughuli za kisiasa na sasa yanalenga zaidi mapambano yake na serikali katika masuala ya mipango miji na turathi.

Share: