Tsh. milioni 400 kupelekwa wilayani nkasi mkoani rukwa kutatua shida ya maji

Aweso ametoa maelekezo hayo wakati akiongea na Wananchi wa Nkasi kupitia simu ya Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, afanye mchakato kuanzia kesho wa kuhakikisha Tsh. milioni 400 zinapelekwa Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa ili kukamilisha mradi wa maji unaolenga kuwaondolea Watu wa Wilaya hiyo shida ya maji.

Aweso ametoa maelekezo hayo wakati akiongea na Wananchi wa Nkasi kupitia simu ya Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi ambaye yupo ziarani Mkoani Rukwa akiwa ameambatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Amos Makalla.

Nchimbi licha ya kumpongeza Aweso kwa kufanikisha kupeleka Tsh. milioni 300 za mradi wa maji Nkasi akataka kujua Tsh. milioni 400 zilizosalia zinapelekwa lini ili kukamilisha mradi .

Aweso amesema “Mh Rais alishatupa maelekezo kwamba yeye ni Mama na asilimia kubwa ya wanaoteseka na changamoto za maji ni akina Mama, hataki kusikia Watu wanateseka , Chama kimefika kimetoa Mil 300 lakini kuna Tsh. milioni 400 zinatakiwa zitolewe, Jumatatu namuelekeza hizo milioni 400 zote zitoke ziende zikakamilishe mradi”

“Nakuhakikishi Mh. Katibu Mkuu, Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo katika kuhakikisha dhamira ya kumtua Mama ndoo kichwani inatekelezeka na Ilani ya CCM inatekelezeka”





Share: