Tra na thrdc yazindua kitabu cha muongozo wa kodi kwa azaki

TRA itaendelea kushirikiana na THRDC na wadau wake wengine kuhakikisha kuwa makundi yote ya AZAKI yanafikiwa

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) wamezindua kitabu cha mwongozo kuhusu kodi kwa Mashirika Yasiyojiendesha kwa Faida Tanzania.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo jijini Dodoma Kamishna wa Kodi za Ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Alfred Mregi amesema kuwa dhamira ya TRA ni kufanya kazi na wadau wote katika kuhakikisha kwamba kila mtu anatimiza wajibu wake katika kulipa kodi.


“TRA inatambua jukumu la Azaki katika kulipa kodi zote za kisheria, niwahakikishie kuwa tutaendelea kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii,’’ alisema Bwana Mregi.

Mregi aliongeza kuwa, kiwango cha uelewa wa masuala ya kodi kimeendelea kukua kwa Mashirika Yasiyojiendesha kwa Faida hapa nchini.

“Taarifa zetu zinaonesha kuwa kiwango cha uelewa wa masuala ya kodi kimeendelea kukua katika kundi hilo kutokana na na uwepo wa mafunzo ya kodi kwa Azaki na matumizi ya kijarida kwa muda mrefu,” alisema Mregi.

Kwa upande wake Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw. Onesmo Ole Ngurumwa, amesema kuwa wazo la kuandaa na kuchapisha mwongozo wa kwanza uliletwa wakati wa mkutano wa wakurugenzi wa Azaki uliofanyika mkoani Mwanza mwaka 2019 na lilipokelewa vema na TRA na Azaki nchini kote.

Alibainisha kuwa, asasi hizo zina mchango mkubwa kwa jamii kwani zinachangia asilimia 40 ya huduma kwenye sekta ya elimu huku kwenye sekta ya afya zikichangia asilimia 50 na kwenye sekta nyingine zikiwemo maji, miundombinu, kilimo na ustawi wa jamii.

“TRA itaendelea kushirikiana na THRDC na wadau wake wengine kuhakikisha kuwa makundi yote ya AZAKI yanafikiwa,” amesema


Naye Mjumbe wa Baraza la Taifa la Asasi za kiraia (NaCongo), Bi. Penina Manyanki amesema kwamba, kitabu hicho kimekuja wakati muafaka kwani hata wale ambao hawajasomea masuala ya sheria wataweza kuelewa kodi zinazotakiwa kulipwa badala ya kuwatafuta wanasheria wawatafsirie sheria hizo.

Kitabu cha Muongozo wa Kodi kwa Azaki kitaondoa malalamiko ya asasi za kiraia kwani wengi watapata uelewa wa kutosha kuhusu kodi wanazotakiwa kuzilipa kwa mujibu wa sheria.

Share: