Tanzania yajifunza mfumo wa fedha kuendesha minada ya madini

Bangkok Ikiwa katika maandalizi ya kurejesha Minada ya Kimataifa ya Madini ya Vito na kuhakikisha inafanyika kwa tija, Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo umeendelea kujifunza kuhusu uendeshaji wa minada nchini Thailand na safari hii umejikita zaidi katika Mfumo wa uwezeshaji kifedha kwa wazalishaji wakati wa kusubiri minada.

Ujumbe huo umejifunza kuhusu uwezeshaji kifedha kwa wazalishaji wa madini ya vito kutoka kampuni ya Delgatto Capital DMCC yenye makao makuu yake nchini Marekani inayofanya kazi kwa kushirikiana na kampuni ya Bonas Group inayoendesha minada ya madini ya vito nchini humo.

Kampuni ya Delgatto imekuwa ikiwawezesha wachimbaji kupata fedha wakati wakingoja kufanyika kwa minada ili kuzalisha malighafi ambazo zinaingizwa katika minada bila kusitisha shughuli za uzalishaji na wakati huo wachimbaji wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji.

Aidha, kampuni hiyo imeanzisha huduma ya uwezeshaji kifedha katika siku za karibuni ili kujibu changamoto za wazalishaji wenye mitaji midogo waweze kuendelea kumudu gharama za uzalishaji wakati wakisubiri minada kufanyika.

Akizungumzia uzoefu huo, Naibu Katibu Mkuu Mbibo amesema ni nafasi nyingine kwa Tanzania kufahamu na kujifunza kuhusu mifumo mbalimbali inavyotumika katika uendeshaji wa minada hiyo hususan namna ambavyo wachimbaji wanaweza kushiriki na kuwezeshwa kifedha kupitia taasisi nyingine kwa ajili ya kuzalisha malighafi ya kulisha minada hiyo na kutumia nafasi hiyo kuwaalika watendaji wa kampuni hiyo kutembelea Tanzania.

"Hiki tulichojifunza leo ndicho tunachokitafuta kwa sababu wachimbaji wetu bado wana changamoto ya mitaji katika kuendesha shughuli zao, uzoefu wa kukutana na kampuni inayowawezesha wachimbaji wa vito vya thamani kupata fedha za kuzalisha malighafi wakati wakisubiri minada kufanyika ni jambo la muhimu kwetu na tunaiona ziara hii ni ya mafanikio," amesema Mbibo.

Naye, Mkurugenzi wa Kanda wa Kampuni hiyo Rajiv Jain ameishukuru Wizara kumwalika ili kuanzisha ushirikiano wa kibiashara na Tanzania na kueleza kuwa, amefurahishwa na ujumbe wa Tanzania kutembelea kampuni ya Bonas Group

Share: