Tanzania na kenya wafikia muafaka huduma ya usafiri wa ndege

TCAA kupitia taarifa yake iliyotelewa na Hamza Johari, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Tanzania imesitisha zuio hilo kufuatia nchi ya Kenya kubadili maamuzi yake.

Mzozo wa kibiashara katika ya Tanzania na Kenya umemalizika baada ya mamlaka za anga za Kenya kuruhusu Shirika la ndege la Tanzania kuendelea na safari zake kati ya Nairobi na Dar es Salaam na shughuli za kusafirisha mizigo kati ya nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Usalama wa anga Tanzania(TCAA), mamlaka za Kenya zimeruhusu Shirika hilo kutumia anga yake kuanzia Januari 16, 2024.

Hii ni baada ya Kenya kukiuka kifungu cha 4 cha Mkataba wa Makubaliano ya Huduma za Ndege, kati ya Tanzania na Kenya uliotiwa saini Novemba 24, 2016 Nairobi, Kenya, kwa kukataa kutoa kibali kwa Air Tanzania cha kuendesha safari za mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Nairobi na mataifa mengine.

Hatua hiyo, iliwalazimu Tanzania nao kusimamisha safari za Shirika la Ndege la Kenya Airways, ndani ya anga la Tanzania.

Katika utetezi wa maamuzi yake, Tanzania ilisisitiza kuwa ilikuwa inajibu uamuzi wa Mamlaka ya Anga ya Kenya kukataa ombi la Tanzania kufanya shughuli zote za ndege za mizigo na Air Tanzania Company Limited chini ya Haki ya Tano ya Haki za Trafiki kati ya Nairobi na nchi tatu.

Hata hivyo, TCAA kupitia taarifa yake iliyotelewa na Hamza Johari, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Tanzania imesitisha zuio hilo kufuatia nchi ya Kenya kubadili maamuzi yake.

"Tuna imani kuwa uamuzi huu utaboresha huduma za usafiri wa anga na kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Kenya," Johari alieleza kwenye taarifa yake.

Mzozo wa kibiashara baina ya nchi hizo wanachama hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliwaibua Mawaziri wanaoshughulika na mambo wa pande zote mbili.

Kwa pamoja, January Makamba wa Tanzania na Musalia Mudavadi waliazimia kumaliza mgogoro huo ndani ya siku tatu.

"Nimezungumza na Mudavadi na tumekubaliana kuwa mzozo huu usiendelee, kwa kutumia mamlaka husika, tunategema kumaliza mgogoro huu ndani ya siku tatu zijazo,”aliandika Makamba kwenye ukurasa wake wa X.

Kwa kawaida, Usafiri wa anga siku zote unaongozwa na haki za utendaji, ambazo ni;

-Haki ya kampuni ya ndege kupita katika anga ya nchi nyengine bila kutua.

-Haki ya ndege kusimama katika nchi nyingine kwa ajili ya kupata huduma nyengine kama vile za kiufundi, kuongeza mafuta bila kubeba au kushusha abiria au mizigo.

-Ndege ya taifa moja inaruhusiwa kupeleka abiria, na mizigo kutoka katika nchi ya uraia wake.

-Kampuni ya ndege inaruhusiwa kuwachukua na kuwasafirisha abiria, barua, na mizigo kutoka nchi ambayo uraia wa ndege hiyo inamiliki.

-Pia ina haki ya kuchukua abiria na mizigo inayopelekwa katika eneo la taifa jengine la tatu na kuwashusha abiria, na mizigo wanaotoka katika eneo lolote kama hilo.

Share: