Tanzania na drc kuuziana mahindi

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamuhuri ya Democrasia ya Congo kwa pamoja wamesaini mkataba wa mauziano ya mahindi tani laki 500,000 ili kuwasaidia wananchi wa DRC kupata chakula cha kutosha na chenye uhakika.

Mkataba huo uliosainiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya ChakuIa (NFRA) na kampuni ya Quincy iliopo jimbo la Katanga,nchini DRC unaonyesha awamu ya Kwanza itaondoka na tani 200,000 na awamu nyingine watamalizia tani 300,000.


Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,Gerald Mweri, amesema wameanza ushirikiano huo wa biashara ya mazao,kama moja ya mkakati waliouweka kwa ajili ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula nchini na barani Afrika kwa ujumla.

"Tumeanza kuwauzia tani hizo za mahindi,tuna akiba ya chakula katika maghala yetu na tayari tumefungua vituo 14 vya kukusanyia mazao hapa nchini,"amesema Mweri.

Amefafanua kwa kusema,serikali imetenga sh bilioni 300 Kwa ajili ya uwekezaji wa kununua mazao ya chakula tani 300,000,ambapo msimu unapoanza NFRA itaanza zoezi la ukusanyaji wa mazao ya chakula.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NFRA DK Andrew Komba amesema msimu unaoanza Julai Mosi,wanaanza ukusanyaji wa mazao ya chakula kama Mahindi,Mpunga na mazao mengine.

Amesema wamejipanga kuhakikisha taifa linakuwa na akiba ya kutosha ya chakula na kuongeza kiwa wananchi wasiwe na wasiwasi wowote kuhusu chakula.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Quincy kutoka Congo, Yuma Gerard Jesse ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kukubali kutia saini ya mkataba wa kuuziana mazao ya chakula.

Katika hatua nyingine Gavana wa Jimbo la Katanga Jacques Kyabula Katwe amesema amekuja Tanzania ili kuonyesha kuwa wamekubali asilimia 100 kununua mazao kwa ajili ya chakula.

Share: