
Inakadiriwa kuwa Tanzania ina hifadhi ya takribani tani 58,500 za urani ambazo tayari zimethibitishwa, huku tafiti zaidi zikiendelea. Bila shaka, haya yote yanazidi kuimarisha matumaini kuwa urani inaweza kuwa msingi wa mabadiliko ya nishati nchini.
Ni kauli nzito ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa mwishoni mwa wiki wakati wa kumuapisha Mkurugenzi mtendaji mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange.
"Ndani ya nchi yetu Mungu ametubariki uraniamu (urania). Ni vyema kusimamia ule mradi wetu kule Namtumbo, wale wawekezaji waanze kazi sasa tufaidike na rasilimali ile."
Kauli hiyo haikufichua tu msimamo wa kisera wa taifa, bali ilidhihirisha pia utashi wa juu wa kisiasa wa kuanza safari ya kuzalisha nishati ya nyuklia kwa kutumia madini ya urani yanayopatikana nchini humo.
Mradi wa Mkuju River uliopo Namtumbo mkoani Ruvuma ndiyo unatazamwa zaidi, lakini maeneo mengine kama Bahi, alapo, Minjingu, Mbulu, Simanjiro, Ziwa Natron, Manyoni, Songea, Tunduru, Madaba, na Nachingwea nayo yamegundulika kuwa na madini haya muhimu.