
Serikali imezitaka kamati za ulinzi na usalama kwenye mikoa yote nchini kuwachukulia hatua kali wale wanaotoa mikopo bila kuwa na leseni, pamoja na kuwanyang’anya leseni hizo wote wanaotoa mikopo bila kuzingatia masharti na kuwaumiza wananchi.
Mikopo hiyo, ambayo imepachikwa majina mengi ikiwemo kausha damu, komandoo, pasua moyo, kichefuchefu na mengine mengi, imekuwa ikitajwa kuwa chanzo cha kufilisika, kujiua, kuvunjika kwa mahusiano na kusababisha magonjwa ya akili baada ya wakopaji kushindwa kuilipa kutokana na masharti magumu.
Wakati mikopo hiyo ikiendelea kutolewa, leo Jumatatu, Februari 17, 2025, Serikali imejitokeza tena kutoa maagizo ya kupambana na tatizo hilo. Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, wakati wa ufunguzi wa jengo la ofisi ya Hazina Ndogo ya Mkoa wa Geita, akisema wimbi la mikopo umiza limeendelea kuwatesa wananchi.
Akisoma hotuba ya Dk Mwigulu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, amesema kumekuwa na changamoto katika sekta ya fedha, ikiwemo taasisi na watu binafsi kutumia mwanya wa uhitaji wa pesa miongoni mwa wananchi na kuwatoza riba kubwa kiasi cha kuwafilisi.
“Mikopo hii inajulikana kama mikopo umiza, kausha damu, chuma ulete, mikopo kuzimia na mengine mengi. Nitoe onyo kwa watu binafsi na taasisi zinazojihusisha na utoaji wa mikopo ya aina hii kuacha mara moja kwa kuwa jambo hili linarudisha nyuma wananchi na kuwaingiza kwenye lindi la umaskini,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kuwa na nidhamu ya fedha, ikiwemo kukopa kwa ajili ya uzalishaji mali badala ya matumizi ya kawaida, na kukopa kwenye taasisi zinazotambulika.
Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kati ya Julai 2019 na Machi 2021, malalamiko 195 yalipokelewa kuhusu mikopo umiza. Kati ya malalamiko hayo, asilimia 66 yalitoka kwa walimu (walio kazini na wastaafu), asilimia 12 yalitoka kwa wafanyabiashara, na asilimia 8 yalitoka kwa askari.