Kutokana na mabadiliko hayo, iliibuka sintofahamu baada ya madaktari bobezi kuyalalamikia wakidai kutoshirikishwa huku wamiliki wa hospitali binafsi wakieleza kutoyaafiki.
Serikali ya Tanzania imesitisha bei mpya za kitita cha matibabu kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) huku ikitangaza kuunda kamati huru itakayofanya mapitio ya maboresho yaliyofanyika.
Bei hizo mpya zilizopangwa kuanza kutumika kuanzia Januari mosi, 2024 zimesitishwa hadi itakapotangazwa tena.
Hatua hiyo inatokana na tishio la hospitali binafsi kusitisha huduma za matibabu kwa wenye kadi za NHIF na hivyo kulazimu mazungumzo ya mezani na waziri mwenye dhamana ya afya, Ummy Mwalimu.
Desemba 18, 2023 NHIF ilifanya mapitio ya kitita cha mafao kwa mwaka 2023, ambayo kwa mujibu wao yalilenga kuongeza au kupunguza gharama katika baadhi ya huduma, ili kuendana na bei halisi ya soko.
Kutokana na mabadiliko hayo, iliibuka sintofahamu baada ya madaktari bobezi kuyalalamikia wakidai kutoshirikishwa huku wamiliki wa hospitali binafsi wakieleza kutoyaafiki.
Uamuzi huo umefikiwa jana Alhamisi, Januari 4, 2024 baada ya mkutano wa ndani kati ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na wawakilishi wa wamiliki wa hospitali binafsi wakiwamo Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), Chama cha Wamiliki wa Vituo vya Aafya Binafsi Tanzania (APHFTA) na Bakwata.