Serikali kuwawezesha vifaa vijana wahitimu wa fani ya uongezaji thamani madini

Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha panakuwepo na mwendelezo wa ujuzi na utaalam wanaopata wanafunzi wa fani ya jemolojia ambapo imepanga kuwapatia bure vifaa vya kuwawezesha kujiajiri na kuongeza thamani ya madini.

Hayo yamesemwa leo tarehe 17 Novemba, 2023 Jijini Arusha na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb) alipotembelea Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kinachotoa mafunzo ya Astashahada na Stashahada ya fani za Jemolojia na uongezaji wa thamani madini.

" Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa ziarani Mkoani Lindi, alituelekeza Wizara ya Madini kuhakikisha tunaweka mkazo katika uongezaji thamani madini. Katika kutekeleza hilo, Kituo hiki ni muhimu sana katika kuwezesha Serikali kufanikisha uongezaji wa thamani madini nchini." amesema Mhe. Mavunde 

"Ili kuondokana na changamoto inayowakabili wahitimu wengi wa Kituo cha TGC, kuanzia mwaka ujao wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia Wizara ya Madini itatenga fedha za kuwezesha vifaa kwa vijana wanaohitimu ili waweze kujiajiri na kuwa na mchango katika uongezaji thamani madini nchini." ameongeza Mhe. Mavunde 

Serikali isingependa kuona vijana wanaohitimu katika fani ya Jemolojia na uongezaji thamani madini, wanakwenda kufanya shughuli zingine kwa changamoto kubwa tu ya kukosa mitaji au vifaa vya kuwezesha kutumia ujuzi wao.

Uwezeshwaji wa vifaa kwa vijana hao itakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya kuwezesha vijana kwenye sekta ya madini itayojulikana kama Mining for a Brighter Tommorow (MBT) yenye lengo la kuongeza ushiriki wa vijana kwenye shughuli zote za mnyororo wa thamani wa madini”Alisema Mavunde

Awali, akimkaribisha Mheshimiwa Waziri, Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga alibainisha kuwa Kituo hicho kimedhamiria kuhakikisha kwamba dhamira ya Serikali katika uongezaji thamani madini nchini hususan ya Vito inakwenda kutimia.

Share: