Mhe. Chande aliahidi kuambatana na Mbunge wa eneo hilo ili kusikiliza maoni ya wafanyabiashara walio tayari
Serikali imesema kuwa inatarajia kufungua Ofisi za Forodha katika Bandari ya Nyamisati mkoani Pwani katika Mwaka wa Fedha 2024/25, baada ya tathmini iliyofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuonesha kuwa mazingira yanaruhusu uwepo wa Ofisi hiyo.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibiti, Mhe. Twaha Ally Mpembene, aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kuweka huduma za Wakala wa Forodha katika Bandari ya Nyamisati.
Mhe. Chande alisema kuwa uamuzi wa kuanzisha Kituo cha Forodha eneo hilo unatokana na kukamilika kwa tathmini iliyofanywa na TRA na kujiridhisha na mawanda ya shughuli zinazofanyika katika eneo hilo.
“Serikali itahakikisha mapema mwaka ujao wa fedha, Ofisi ya Forodha katika Bandari ya Nyamisati iwe imekamilika na kuanza kutoa huduma”, alisema Mhe. Chande.
Aidha Mhe. Chande aliahidi kuambatana na Mbunge wa eneo hilo ili kusikiliza maoni ya wafanyabiashara walio tayari kutumia bandari hiyo na pia kuangalia namna bora ya usafirishaji wa bidhaa katika bandari hiyo.