Serikali inaangalia namna ya kufanya upanuzi wa bandari ya dar es salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaangalia namna ya kufanya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam ili kuendana na ongezeko la mizigo inayohudumiwa baada ya baadhi ya wamiliki wa migodi kutoka nchi jirani kuonyesha nia ya kuanza kutumia Bandari ya Dar es Salaam na Kigoma kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho amesema DP World ilianza kazi Aprili 7, 2024 licha ya kuwa TPA inamalizia baadhi ya vitu kabla ya kuachia kila kitu chini ya mwendeshaji huyo. Ameongeza kuwa kilichobakia chini ya TPA ni baadhi ya meli zilizokuwa zimesajiliwa katika mifumo ya TPA ambazo ni lazima wazihudumie.

Mrisho ameeleza hayo leo Juni 3, 2024 wakati Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Ali Possy alipofika Bandari ya Dar es Salaam kuangalia namna shughuli zinazofanyika baada ya DP World kuanza utekelezaji akiambatana na ujumbe kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac).

"Shughuli hazijasimama pamoja na makabidhiano hayo, changamoto kama wadau fulani walizungumza kuhusu mifumo ndiyo hiyo tunayosema transition tunaimarika sana na hiyo mifumo wanayoizungumzia ya DP World, nadhani baada ya muda tutakaa sawa zaidi, kazi zinaendelea, gati zote zimejaa meli na meli zinahudumiwa," amesema Mrisho.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dk Ali Possi amesema wakati watoa huduma hao wakianza kazi, lengo la Serikali ni kuona ufanisi unakua kama ilivyokuwa imetarajiwa.

Itakumbukwa Oktoba 22, mwaka jana Serikali iliingia makubaliano na DP World kupitia mikataba mitatu iliyosainiwa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika bandari hiyo kwa miaka 30.

Share: