Serikali hatua za mwisho upatikanaji wa leseni kubwa

Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuwezesha upatikanaji wa Leseni Kubwa ya uchimbaji madini (Special Mining License - SML) kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sand,inayomilikiwa na kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Strandline,ambayo itapelekea kuanza kwa mradi mkubwa wa uchimbaji madini Tembo katika Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga.

Hayo yameelezwa leo tarehe 20 Februari na, 2024 na Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde alipofanya ziara ya kutembelea sehemu ya eneo la mradi huo iliyopo katika kijiji cha Stahabu, Kata ya Mikinguni Wilayani Pangani-Tanga. "Ni dhamira ya Serikali yetu kuona wawekezaji wakubwa wenye nia njema na Nchi yetu kama hawa wanapewa ushirikiano ili kuwezesha shughuli zao kwa manufaa ya Taifa letu".

"Mradi huu unatarajiwa kuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni 125 ambao unakadiriwa kuishi kwa miaka 20 hadi 25 utatekelezwa katika Vijiji 8 vilivyopo katika Kata za Mikinguni, Mwera, Tungamaa na Bweni Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga.

Nimefurahishwa na utayari wa wananchi wanaoguswa na mradi kupisha kuanza kwa mradi, na kwa kuwa ni hatua muhimu sana kwani itarahisisha kuanza mradi kwa wakati na kuondoa changamoto ya migogoro kati ya wananchi na mwekezaji”Alisema Mavunde

Akizungumza kwa niaba ya Mwekezaji, Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyati Mineral Sand Ltd ambaye anawakilisha Hisa za Serikali, Ndg.Heri Gombera alieleza kwamba mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka 2026 na unatarajiwa kuzalisha tani milioni 8 kwa mwaka ya madini mbalimbali yakiwemo titanium, ilmenite, rutile, zircon na monazite ambayo pamoja na matumizi mengine hutumika pia kuzalisha malighafi za injini za ndege, nyuklia, vifaa vya hospitali na viwanda vya marumaru na rangi.

Share: