Rc chalamila bandari kavu (icd) kusaidia kupunguza msongamano wa mizigo bandarini

mipango mikakati iliyopangwa hapo itaisaidia bandari kupokea shehena kubwa hivyo wapo tayari kushiriana na serikali na kukuza uchumi wa nchi kiujumla.

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila leo Desemba 13, 2023 amekutana na uongozi wa Bandari na viongozi wa Bandari kavu (ICD) kujadili michakato ya kuondosha mizigo Bandarini.

RC Chalamila alisema kwa sasa bandari ya Dar es salaam inapokea mizigo mingi ila miundo mbinu bado ni ileile ya zamani hivyo kusababisha msongamano mkubwa wa bidhaa, magari na makasha bandarini hapo.

Aidha RC Chalamila alieleza sababu ya ongezeko la mizigo zikiwemo sikukuu na likizo kwa watumishi wa meli kwa nchi mbalimbali, "Tupo kipindi ambacho ujio wa meli ni mkubwa sana ikilinganishwa na miundombinu ambayo ndiyo haswa sababu ya Mhe Rais Dkt Samia kuwaza sasa mawazo mapana ya utanuzi wa bandari yetu ya Dar es Salaam."

Vilevile RC Chalamila alisema kutaundwa timu ya pamoja ambayo itayafanyia kazi yale yote waliyokubaliana, na wadau wote waweze kushiriki ili kuongeza ufanisi hivyo kupata majibu ya namna ya kuondoa changamoto hizo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA), Bw. Plasduce Mbossa alisema wastani kwa siku wanapokea meli tano mpaka saba na kupambana kuzitoa zote siku hiyohiyo wakishirikiana na bandari kavu, na kupitia kikao hicho wamejadili namna ya kuongeza ufanisi uondoshaji wa mizigo kwa gharama nafuu, na kuweza kuhudumia nchi jirani.

Kwa upande Mmiliki wa Bandari Kavu ya PMM Dkt Judith Mhina, mipango mikakati iliyopangwa hapo itaisaidia bandari kupokea shehena kubwa hivyo wapo tayari kushiriana na serikali na kukuza uchumi wa nchi kiujumla.

Share: