Rais samia suluhu hassan amesema anataka biashara zifanyike saa 24 kariakoo jijini dar es salaam

RAIS wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo asiwe Waziri wa kukaa ofisini tu bali aende field ili kusikiliza na kuzitatua kero za Wafanyabiashara ambapo pia amesema anataka biashara zifanyike saa 24 Kariakoo Jijini Dar es salaam na hivyo amemuagiza Jafo afanikishe hilo.

Akizungumza leo Julai 05, 2024, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar wakati akiwaapisha Viongozi Wateule, Rais Samia amesema “Nianze na Jafo, ulikuwa Ofisi ya Makamu wa Rais umefanya vizuri lakini nimeona nikutoe nikupeleke biashara kwasababu biashara pilika ni nyingi mno na kuanzia sasa pale ofisini mwenzio alipokuwa anakaa sitaki ukae lakini namuelewa Waziri kwanini alikuwa haendi huko kwa kazi ninayotaka kukupa kwa Mtoto wa kike sio rahisi, kushinda Kariakoo juu chini, chini juu sio rahisi, hiyo kazi nataka uifanye wewe “

“Pia ukarejee Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM inayozungumzia Sekta ya Biashara na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kukua na ukarejee kauli yangu kwenye ufunguzi wa maonesho juzi Sabasaba nimesema Serikali itafanya kila linalowezekana kusikiliza na kutatua changamoto za Wafanyabiashara Nchini na ndio maana nakuambia uwe juu chini Kariakoo”

“Kariakoo ni eneo zuri sana la biashara na eneo muhimu sana la biashara na ndio linalofanya Dar es salaam iitwe kitovu cha biashara kwasababu Mataifa yote yanakuja Kariakoo lakini Kariakoo tumeweka pesa nyingi sana kujenga yale masoko ya Kariakoo na masoko yakimalizika nataka biashara zifanyike saa 24”

“Kwahiyo ukaifanye Kariakoo iwe inatoa huduma saa 24 huku kukiwa na usalama wa biashara na Wafanyabiashara, kwahiyo mtakaa vipi na Jeshi la Polisi mtajipanga vipi, hiyo ni kazi yako lakini nataka Kariakoo pawe na soko la biashara la Kimataifa na kwasababu mwaka huu mwishomwisho tunamaliza yale majengo Wamachinga na wengine walioko pale wataingizwa ndani ya soko”

Share: