Rais dkt. samia ni kielelezo cha mafanikio nchini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amekuwa kielelezo cha mafanikio makubwa yanayofikiwa nchini, hivyokuliwezesha Taifa kuendelea kupata utulivu, maelewano na kasi kubwa ya maendeleo kupitia maono, maelekezo na mipango mbalimbali.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi ameyasema hayo leo (Jumanne, Januari 2, 2024) kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM wa wilaya ya Ruangwa uliofanyika katika Uwanja wa Likangara, Ruangwa ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Abdulrahman Kinana.

Waziri Mkuu ametaja baadhi ya masuala makubwa ya Kitaifa yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani ni pamoja na kuendeleza miradi ya kielelezo na ya kimkakati ukiwemo ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa wa Reli ya Kisasa na madaraja makubwa likiwemo la Kigongo - Busisi ili kukuza uchumi, kuongeza fursa za ajira na kufikia malengo yaliyokusudiwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Waziri Mkuu amesema mafanikio mengine ni kurejesha taswira ya Tanzania katika medani za kimataifa na kuimarisha diplomasia ya uchumi. “Kwa kufanya hivi Mheshimiwa Rais, amefungua fursa mbalimbali ukiwemo uwekezaji, mitaji, masoko ya bidhaa, ongezeko la watalii, kubidhaisha lugha ya Kiswahili na utatuzi wa changamoto za kibiashara na nchi jirani.

Share: