Kwa upande wake mwanafunzi, Amokile Sanga amesema kuwa, mabweni hayo yamekuwa msaada mkubwa kwani wanalala vizuri bila kubanana na ni mabweni bora kwa kuwa yamejengwa kisasa
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya Yakobi iliyopo katika Kijiji cha Limage, Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe, Editor John amesema kuwa kutokana na Serikali kupeleka fedha kwa ajili ya kuongeza mabweni, udahili wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi 105 hadi 433.
Ameyazungumza hayo hivi karibuni wakati akihojiwa na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari (Maelezo) ambapo amesema kuwa, jumla ya shilingi milioni 543 zilipelekwa na Serikali kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu ya elimu kwa ajili ya kidato cha tano na sita ambapo fedha hizo zimeweza kujenga mabweni matatu ya watoto wa kike, madarasa matano pamoja na matundu 14 ya vyoo.
“Tulifanikiwa kutekeleza ujenzi wa mabweni matatu ambayo yamekamilika na wanafunzi wanaishi, madarasa matatu, ofisi moja, matundu 16 badala ya 14 pamoja na samani za ndani ya mabweni ambapo ilitakiwa kununua vitanda vya deka 120 lakini kupitia matumizi mazuri ya fedha hizo, vilinunuliwa vitanda vya deka 180 na badala ya kununua viti 200 na meza 200, imewezekana kununua viti 380 na meza 380, alisema bi. Editor.
Bi. Editor ameongeza kuwa, mnamo mwezi Agosti, 2023 Serikali ilileta tena jumla ya shilingi milioni 130 kwa ajili ya ujenzi wa bweni lingine la wasichana ambalo linakaribia kukamilika. Aidha, ameishukuru Serikali kwa ujio wa fedha hizo kwani sio mara ya kwanza kuwakumbuka, hata kipindi cha kwanza cha kuanzisha kidato cha tano na cha sita, ilipeleka jumla ya shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni ambalo kwa kiasi kikubwa limewasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira bora na wote kufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu.
Kwa upande wake mwanafunzi, Amokile Sanga amesema kuwa, mabweni hayo yamekuwa msaada mkubwa kwani wanalala vizuri bila kubanana na ni mabweni bora kwa kuwa yamejengwa kisasa, ameeleza kuwa taaluma bora huwa inaendana na miundombinu bora hivyo kuongezeka kwa mabweni hayo kumewasaidia kuwa na taaluma bora.