Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema Dira ya maendeleo ya Taifa 2050 itatia mkazo zaidi kwenye Usafirishaji fungamanishi, Sayansi na Teknolojia, Utafiti na maendeleo, Mageuzi ya kidigitali pamoja na uimarishaji wa sekta ya Nishati ili kuhakikisha kuwa mambo hayo yanachochea Tija na ufanisi katika kufikiwa kwa malengo ya dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Akiwa Kisiwani Zanzibar leo Jumatano Disemba 11, 2024 Wakati wa uzinduzi wa Rasimu ya Kwanza ya Dira 2050, Waziri Profesa Mkumbo amesema Vichocheo hivyo vina nafasi kubwa ya kuchochea kasi kwenye utekelezaji wa malengo mengine katika kuhakikisha kuwa dira 2050 inatekelezeka kikamilifu ndani ya muda wa miaka 25 ijayo.
Akizungumzia muundo wa Rasimu hiyo iliyozinduliwa leo, Prof. Mkumbo amesema pamoja na mambo mengine, Dira hiyo itaongozwa na msingi Mkuu wa Utawala, Amani, Usalama na Utulivu kwakuwa mambo hayo ndio msingi na kivutio kikuu cha maendeleo kote duniani hasa katika uwekezaji, ustawi na maendeleo kwa ujumla wake.
Aidha Waziri Kitila Mkumbo katika uzinduzi wa Rasimu hiyo ya kwanza ya Dira 2050 amesema nguzo za Dira 2050 zitakuwa ni Uchumi imara jumuishi na shindani, Uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, Uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.