Mwanzilishi wa amazon jeff bezos anasema atauza hisa nyingine milioni 25 katika kampuni kubwa ya teknolojia

Mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos anasema atauza hisa nyingine milioni 25 katika kampuni kubwa ya teknolojia, yenye thamani ya karibu $5bn (£3.9bn).

Hii inawadia baada ya thamani ya soko la hisa ya kampuni hiyo kufikia rekodi ya juu siku ya Jumatano.

Mnamo mwezi Februari, alitangaza kwamba atauza hisa za Amazon zenye thamani ya karibu $8.5bn.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza tangu 2021 kwa Bw Bezos kuuza hisa za Amazon.

Hisa za kampuni hiyo zimeongezeka kwa zaidi ya 30% mwaka huu kwa matarajio kwamba kuongezeka kwa mahitaji ya teknolojia ya akili bandia (AI) kutaongeza mapato katika biashara yake ya ‘cloud computing’.

Mwezi uliopita, hesabu ya soko la hisa la Amazon ilipanda $2tn kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, bado iko nyuma ya makampuni mengine makubwa ya teknolojia ya Nvidia, Apple na Microsoft, ambayo yote yamevuka $3tn.

Amazon iliripoti mapato makubwa ya robo mwaka mwishoni mwa Aprili, ambayo yalionyesha dau la kampuni kwenye AI ilikuwa likizaa matunda.

Bw Bezos alijiuzulu kama mtendaji mkuu wa kampuni hiyo mnamo 2021 na kwa sasa ndiye mwenyekiti wake mkuu na anasalia kuwa mwanahisa mkuu.

Alianzisha Amazon mwaka wa 1994 katika karakana huko Bellevue, Washington, wakati mtandao ulikuwa bado mchanga.

Kampuni hiyo ilianza kama muuzaji vitabu mtandaoni, na kupigia debe mkusanyiko mkubwa zaidi wa vitabu kwa njia ya kielektroniki duniani.

Tangu wakati huo Amazon imekuwa mojawapo ya makampuni yanayoongoza duniani ya rejareja na ‘cloud computing’.

Pia alianzisha kampuni ya roketi ya Blue Origin, ambayo mnamo mwezi Mei ilituma wateja sita mwisho kabisa mwa anga la mbali.

Bw Bezos ndiye mtu wa pili tajiri zaidi duniani, kwa mujibu wa orodha ya Mabilionea ya Forbes, akiwa na utajiri wa takriban $214bn.

Share: