Msimamo wa ccm kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuwajulisha wadau wote wa elimu na Umma wa Watanzania kuwa kitaendelea kuisimamia Serikali ili kuongeza utoaji wa mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu wenye sifa stahiki.

Kama ambavyo tumeahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi (2020-2025) katika ukurasa wa 131, tutaendelea kuhakikisha wanafunzi wengi wenye uhitaji nasifa wanapata fursa ya kujiunga na elimu na kupata mikopo kama inavyostahili.

Katika kutimiza azma hiyo, Serikali inayoongozwa na CCM iliondoa asilimia kumi ya faini kwa wale wanaochelewa kuanza kurejesha mikopo yao kwasababu mbalimbali.

Pia uamuzi wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kutangaza kuondolewa kwa tozo ya asilimia sita (Value Retention Fee) iliyokuwa ikitozwa kwa ajili ya kulinda thamani ya fedha wakati wa urejeshwaji wa mikopo ya wanufaika, ni ushahidi mwingine wa kuwapunguzia makali ya maisha vijana wetu waliohitimu elimu ya juu nchini.

Kadhalika, Serikali ya CCM imeongeza pesa ya kujikimu, 'boom' toka Shilingi8,500/- hadi Shilingi 10,000/- kwa siku. Tuna uhakikishia Umma wa Watanzania kuwa CCM itaendelea kuisimamia Serikali kutenga na kutoa pesa hizi za kujikimu na gharama nyingine kwa wanufaika wengi zaidi wenyesifa stahiki.

Maoni ya baadhi ya watu juu ya kuondolewa kwa fedha za kujikimu hayatazingatiwa kwani hakuna haja ya kumpangia matumizi ya fedha mtu mzima.

Share: