Mivutano baina ya watumishi na wakopeshaji wasio rasmi huathiri utendaji katika sehemu za kazi

Watumishi wa umma wilayani Kibondo mkoani Kigoma, wametakiwa kuacha tabia ya kujihuisha na ukopaji wa fedha katika taasisi zisizo rasmi ambazo maranyingi huwa na riba kubwa na kusababisha migogoro wanaposhindwa kulipa kwa wakati.

Akizungumza na timu ya wataalamu wa fedha kutoka wizara ya fedha, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Dkt. Gabriel Chitupila, alisema kuwa mivutano baina ya watumishi na wakopeshaji wasio rasmi huathiri utendaji katika sehemu za kazi na kuhatarisha utumishi wa mkopaji.

Dkt. Chitupila alisema kuwa hali hiyo husababisha kushusha ari ya watumishi kufanyakazi kutokana na muda mwingi wakijikuta wanakimbizana na wakopeshaji hasa pale mkopo unapokuwa mkubwa na kushindwa kulipa hivyo akawasihi kama kuna ulazima wa kukopa wazitumie taasisi ambazo zimesajiliwa ili wapate huduma yenye uhakika isiyo kandamizi.

“tatizo la mikopo “kausha damu” lipo na linawakumba hadi watumishi wa umma hasa walimu, unakuta mwalimu hakai ofisini akiogopa kutafutwa na wakopeshaji au kulazimika kutoroka katika kituo chake cha kazi kwenda kufanya vibarua sehemu nyingine ili pate hela za kulipa deni na kusababisha wanafunzi kukosa haki yao ya msingi ya kufundishwa, nitoe rai wenye tabia hiyo waache mara moja” alıonya Dkt. Chitupila.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Agrey Magwaza, aliwahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii na Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha ngazi ya Halmashauri kufuatilia na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kifedha ili kuwasaidia kuwa na uelewa juu ya masuala mbalimbali ya huduma hizo.

" Maafisa Maendeleo ya Jamii na Waratibu wa Huduma za Kifedha katika halmashauri tufahamu kuwa kipimo chetu sisi watumishi wa umma ni namna tunavyo wahudumia wananchi na kuona wanavyoridhika na huduma kwa kulimaliza tatizo la kuwepo kwa watoa huduma wanaoweka riba kubwa na kukiuka sheria za nchi, hicho ndicho kitakuwa kipimo chetu cha utumishi". Alisema Kanali Magwaza.

Aidha, Magwaza alisema kuwa ni rahisi sana mtu kukopo wakati anaona riba ni kubwa lakini akianza kukatwa fedha ndio anaona fedha ni kubwa na mwishowe anajuta.

"Mtu anaona riba ni kubwa lakini anaona sawa tu na anapoanza kukatwa fedha zake ndipo anakunywa na msongo wa mawazo na hatimaye mtu huyo anapoteza mwelekeo". Alisisitiza Kanali Magwaza.

Share: