Wakandarasi hao , NAMIS Corporate Ltd na Central Electrical International Co, wametakiwa kuongeza nguvu kazi na upatikanaji wa vifaa kwa wakati
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini katika Wilaya za Nachingwea, Nanyumbu, Masasi na Tandahimba kukamilisha miradi yao ifikapo Desemba 31, mwaka huu.
Pia amewaelekeza kuhakikisha ubora, weledi na kukamilika kwa wakati miradi yote wanayoisimamia ili wananchi wapate huduma kwa muda uliopangwa.
“Nishati ni kila kitu, usalama, uchumi, siasa, afya na maeneo mengi,
hivyo, jukumu la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni kuhakikisha kuwa wanawapatia wananchi umeme ili waweze kutimiza malengo yao,” amesema Balozi Kingu.
Amesema hayo katika kikao chake na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya nishati vijijini katika Mkoa wa Mtwara ambapo amewataka watendaji wa REA na TANESCO kuwafuatilia kwa karibu kuhakikisha kuwa lengo la kuvifikia vijini vyote ifikapo Juni 30, 2024 linafikiwa.
Wakandarasi hao , NAMIS Corporate Ltd na Central Electrical International Co, wametakiwa kuongeza nguvu kazi na upatikanaji wa vifaa kwa wakati ili ifikapo Novemba 30, 2023 vijiji vyote walivyopangiwa kimkataba viwe vinawaka umeme.
Amewaagiza kutumia vifaa vinavyozalishwa na kupatikana katika viwanda vya ndani ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuagiza nje vile tu ambavyo havipatikani nchini.
Ametaka kikao cha tathmini kifanyike Desemba Mosi mwaka huu na wakandarasi hao na kuona kama wako katika muda uliopangwa na endapo kuna changamoto waone namna bora ya kuzitatua kwa pamoja.
Pia amewataka Wakandarasi kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa kazi zao kila wiki ili kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa miradi hiyo.