Mheshimiwa paul christian makonda ametangaza kuja na operesheni ya kurejesha haki kwa wakazi wote wa arusha

Mkuu wa Mkoa alitaja vipaumbele vyake vitano alivyokuja navyo Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Paul Christian Makonda ametangaza kuja na Operesheni ya kurejesha Haki kwa wakazi wote wa Arusha waliotapeliwa ama kunyang'anywa Haki zao ikiwemo kwa walioporwa ardhi mengineyo.

Akizungumza wakati wa Harambee ya Ujenzi wa Kanisa Katoliki Usa River, Mhe. Makonda amewaambia waumini wa kanisa hilo kuwa hiyo ndiyo Kazi miongoni mwa nyingi anazoamini kuwa anatakiwa kuzifanya kikamilifu kama Kiongozi wa wananchi hasa wanyonge wanaohisi kutosikilizwa vilio vyao kutokana na kuporwa haki zao na wenye Mamlaka ama fedha nyingi kuwazidi.

Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema Operesheni hiyo itafanyika punde tu mara baada ya kuhitimika kwa sherehe za siku ya wafanyakazi, zinazotarajiwa kufanyika Kitaifa Mkoani Arusha kwenye Uwanja wa Michezo wa Sheikh Amri Abeid.

Kuhusu Tarehe Rasmi ya Kuanza kwa Operesheni hiyo, Mhe. Paul Christian Makonda amesema ratiba itatangazwa na Ofisi yake mwanzoni mwa mwezi Mei Mwaka huu.

Wakati wa Ukaribisho wake na makabidhiano ya Ofisi, Mkuu wa Mkoa alitaja vipaumbele vyake vitano alivyokuja navyo Arusha na miongoni mwake ilikuwa ni pamoja na kuwa sauti ya Wanyonge walionyang'anywa haki zao na Mali zao mbalimbali, Zoezi ambalo alidai linafanywa na wenye fedha na wenye Mamlaka wakishirikiana na watumishi wasiokuwa waaminifu serikalini.

Share: