Mhe. katambi abainisha mikakati ya serikali kukuza ustawi wa watu wenye ulemavu

Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imefufua vyuo vya Watu wenye Ulemavu kwa kutumia Tsh. Bilioni 3.4.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Watu wenye Ulemavu ili kukuza ustawi wa kundi hilo katika kuchochea shughuli za maendeleo.

Ameeleza hayo katika tamasha la kimataifa la familia yenye furaha la Watu wenye Uziwi na usikivu hafifu, lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo tamasha hilo lilihusisha pia mshindano la kumsaka mrembo, mtanashati pamoja na mwanamitindo bora duniani mwenye Uziwi.

Aidha, Mhe. Katambi amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapenda na kuwajali Watu wenye Ulemavu na ndio maana serika anayoiongoza imeunda wizara mahususi ili kusimamia watu wenye ulemavu.

Amebainisha kuwa Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imefufua vyuo vya Watu wenye Ulemavu kwa kutumia Tsh. Bilioni 3.4 kukarabati miundombinu ambayo imechakaa katika vyuo 6.

Pia ameeleza kwa mwaka huu wa fedha 2023-2024 serikali imetenga Bil. 3 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vipya vitatu vya ufundi stadi ili kuongeza udahili wa vijana wenye Ulemavu kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Vile vile, katika kuimarisha utambuzi wa mapema wa watoto wenye Ulemavu, serikali imeandaa mwongozo wa utambuzi wa mapema na afua staki kwa watoto wenye Ulemavu.

Sambamba na hayo, amesema kuwa Serikali imeendelea kuwawezesha Watu wenye Ulemavu kiuchumi kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Share: