Mhe. dkt. nchemba ateta na balozi mpya wa umoja wa ulaya jijini dar es salaam

Balozi mpya wa Umoja wa Ulaya, Mhe. Christine Grau, alisifu mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea nchini.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa kutenga zaidi ya euro milioni 703 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha miaka 7 kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2027.

Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi mpya wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe. Chistine Grau aliyefika kujitambulisha rasmi.


Mhe. Dkt. Nchemba alisema awamu ya kwanza ya kipindi cha miaka 4 ilitengewa zaidi ya euro milioni 426 ambapo mpaka sasa Umoja huo umetoa zaidi ya euro milioni 373 ambazo zimeelekezwa katika miradi kadhaa ikiwemo uchumi wa buluu, ujenzi wa miji ya kisasa, upatikanaji wa mitaji, utawala wa fedha, upatikanaji wa mitaji kwa sekta binafsi, usawa wa kijinsia na mradi wa kuendeleza masuala ya kidigiti.

Aliiomba EU kuangalia uwezekano wa kutumia sehemu ya fedha, zaidi ya euro milioni 200 zitakazotumika katika awamu ya pili ya program hiyo itakayoanza mwakani kitumike kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya barabara ya kutoka Mikumi hadi Kidatu yenye urefu wa kilometa 35 ili kuchochea uchumi na maendeleo ya wakazi watakaonufaika na barabara hiyo.

Kwa upande wake, Balozi mpya wa Umoja wa Ulaya, Mhe. Christine Grau, alisifu mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea nchini kupitia kwa ungozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya MUungano wa Tanzania, yaliyoifanya Tanzania kuendelea kuwa imara na kuvutia uwekezaji na mitaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Aidha, Mhe. Balozi Grau aliarifu kuwa majadiliano ya awali ya ushirikiano mwingine wa miaka 7 unaotarajiwa kuanza mwaka 2028 hadi 2034 yataanza rasmi mwakani 2025.

Mhe. Balozi Grau aliipongeza Tanzania kwa kuridhia na kusaini mkataba mpya wa ushiriakiano kati yake na Umoja huo ujulikanao kama SAMOA ambao pamoja na mambo mengine utaiwezesha Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya kuendelea kufanyakazi zake nchini.

Share: