Mhe. chande atoa rai kwa taasisi za umma kuhusu matumizi ya mfumo wa nest.

Taasisi za ununuzi za umma nchini zimetakiwa kutumia mfumo wa Kieletroniki wa ununuzi wa Umma (NeST) katika kuchakata ununuzi wake ili kuisaidia serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika katika miradi mbalimbali.

Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande alipokuwa akifungua mafunzo ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko kupita mfumo huo, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam.

“Taasisi zote ambazo hazitatumia mfumo huo zitaadhibiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,” Alisema Mhe. Chande.


Alisema kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, alitoa waraka unaowataka wazabuni na taasisi nunuzi kufanya ununuzi wote ikiwemo kuwasilisha malalamiko au rufaa zao kupitia mfumo huo wa kieletroniki.

“Kwa kuwa shughuli zote za ununuzi zinatumia mfumo kumeonekana kuwa na umuhimu mkubwa wa kazi za kushughulikia malalamiko nazo zifanyike kupitia mfumo huo huo ambao umeweka Moduli mahsusi kwa ajili ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya Wazabuni,” alisema Mhe. Chande.

Aidha, aliitaka Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kwa kushirikiana na PPRA kuhakikisha kuwa inatoa uelewa/mafunzo ya kutosha kuhusu Moduli hiyo mpya.

“Naagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) mhakikishe mnasimamia vyema matumizi ya NeST ili kila taasisi ya serikali iutumie mfumo huo. Kwa kufanya hivyo, taasisi zitakuwa zinatekeleza matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma,” alisisitiza Mhe. Chande.

Vile vile, aliitaka Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) ihakikishe kuwa wataalamu wa ununuzi na ugavi wanasajiliwa na kufanya majukumu yao kwa weledi.


“PPAA hakikisheni mnashirikiana na PSPTB katika maamuzi mnayotoa ili PSPTB waweze kuwachukulia hatua stahiki wataalamu wa ununuzi na ugavi wanapokiuka maadili ya taaluma yao,” alisema Mhe. Chande.

Alitoa wito kwa wazabuni au wafanyabiashara wanaofanya kazi mbalimbali kuwasilisha malalamiko yao kwa kuzingatia muda ulioainishwa kisheria ili ziweze kushughulikiwa kwa wakati.

Mhe. Chande alitoa rai yake kwa washiriki wa mafunzo hayo kutumia vizuri muda wao huo ili waweze kuuelewa Mfumo na kuwafundisha wengine ambao hawakupata nafasi hiyo.

Naye Katibu Mtendaji wa (PPAA) Bw. James Sando alisema Mamlaka imeweza kushughulikia jumla ya mashauri 129 katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaliyotakana na michakato ya Ununuzi wa Umma.


Alisema Mamlaka ya Rufani imeweza kudhibiti utoaji wa tuzo kwa wazabuni ambao walipendekezwa kupewa zabuni bila kuwa na sifa stahiki.

“Mamlaka ya Rufani ilizuia utoaji tuzo kwa wazabuni 27 wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika,” alisema Bw Sando.

Aidha alisema asilimia 23 ya mashauri 129 yaliyosikilizwa yalibainika kuwa na kasoro mbalimbali katika mchakato wake wa ununuzi.

Alisema serikali ingeweza kupoteza kiasi zaidi ya shilingi 543.038 bilioni kwani tuzo za zabuni zingetolewa kwa wazabuni wasiokuwa na sifa za kutekeleza miradi ya maendeleo.

Share: