Malalamiko ya wananchi msimbati yapelekea dkt. biteko kumuondoa meneja mawasiliano tpdc

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza kuondolewa kwa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutokana na kushindwa kutoa taarifa mbalimbali na kutofanya mikutano na wananchi wanaozunguka miradi ya Gesi Asilia ikiwemo dharura zinazotokea katika Mkuza wa Bomba la Gesi.

Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo tarehe 14 Novemba, 2023 wakati aliposimama katika Kijiji cha Msimbati wilayani Mtwara, Mkoa wa Mtwara ili kuzungumza na wananchi akiwa anatokea kukagua visima vya kuzalisha na mitambo ya kuchakata Gesi ya Mnazi Bay iliyopo katika Kata ya Msimbati wilayani humo.

Wananchi wa Kata ya Msimbati walimweleza Dkt.Biteko kuhusu changamoto walizonazo ikiwemo barabara, kituo cha afya, kutopata fedha zozote kutokana na kazi za uzalishaji wa uchakataji Gesi Asilia unaofanyika kwenye kijiji hicho na kutopata taarifa mbalimbali za mradi ikiwemo zinapotokea changamoto kwenye bomba la Gesi Asilia.

Share: