Kila mtu anawajibu wa kusimamia fedha za utekelezaji wa miradi - rc senyamule

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amesema kila mmoja ana wajibu wa kusimamia kikamilifu fedha za miradi ya maendeleo. 

Mhe. Senyamule ameyasema hayo wakati akiongea na wananchi wa Kijiji cha Ng’hambi Kata ya Ng’hambi wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Kimakakati na kuongea na wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa tarehe 17 Januari 2024.

Akizungumza na wananchi hao Senyamule amesema kila wananchi ana haki na wajibu wa kusimamia fedha zinazoletwa kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi Katika Mkoa wa Dodoma ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kuweka nguvu kazi katika usimamizi wa miradi hiyo.

“Wananchi wanahaki ya kusimamia kikamilifu fedha za miradi kwa kuhakikisha matumizi ya fedha hizo yazingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili kuhakikisha kukamilika miradi ya kipaumbele katika mazingira yetu ya kazi.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ana nia nzuri ya wananchi wake ili kuondoa changamoto na kuzitatua na ndio sababu miradi inaletwa kwetu, kazi yetu ni kuhakikisha inakamilika ipaswavyo” amesema Senyamule.

Pia Mhe Senyamule amesisitiza suala la kutunza mazingira ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kukemea suala la wazazi wanaosababisha watoto wasifike shule na kuwataka wapeleke watoto shule kwa wakati na mzazi atakaehusika na uzembe wa aina hiyo atatozwa faini ya laki mbili.

Vile vile Mhe. Senyamule ametembelea ujenzi wa Mradi wa Daraja la NMB Mpwapwa linalogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 599, ujenzi wa Nyumba mbili za walimu katika shule ya sekondari Ng’hambi kupitia mradi wa Sequip ambao ulipokea kiasi cha shilingi Milioni 95 na Mradi wa ofisi na madarasa kwa kutumia "force account" ilipokea kiasi cha shilingi Milioni 45 kwaajili ya shule ya msingi mazae.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo amesema kujenga miradi kwa kutumia force account kunapunguza gharama na inasaidia fedha zilizobakia kutumika kwa matumizi mengine na ubora wa Elimu unachangia kwa makundi matatu kwanza mwanafunzi wenyewe, wazazi na walezi kuhakikisha mtoto anasoma na kundi la Walimu na ndio sababu Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuleta miradi jirani ili kuzidi kuongeza huduma bora za walimu.

Share: