Katibu mkuu wa wizara ya madini akutana na  maafisa madini wakazi wa mikoa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa nchini kuongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli, kutatua migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini sambamba na kuongeza kasi kwenye udhibiti wa utoroshaji wa madini ili Sekta ya Madini iendelee kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Mahimbali ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma kwenye kikao chake na maafisa madini wakazi wa mikoa nchini chenye lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha Sekta ya Madini hasa katika maeneo ya ukusanyaji wa maduhuli na kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini.

Amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ana matarajio makubwa sana kwenye Sekta ya Madini hivyo ni vyema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kufanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za madini kupitia mapato ambayo yanatumika kuendeleza Sekta nyingine muhimu kama uboreshaji wa miundombinu, afya, elimu n.k

Amesisitiza kuwa ni vyema maafisa madini wakazi wa mikoa wakaweka nguvu kwenye ukusanyaji wa maduhuli na kuvuka lengo la makusanyo linalowekwa na Serikali kila mwaka.

Share: