Kamati ya pic yaitaka tanesco na trc kulinda miundombinu ya treni ya kisasa (sgr)

Amesema TANESCO watashirikiana na TRC kuhakikisha miundombinu hiyo inatunzwa na kutumia wataalamu wa ndani ambao wamepatiwa mafunzo maalum

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imeliagiza Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na Shirika la Reli Nchini (TRC), kutunza Miundombinu ya mradi wa Treni ya Kisasa kwa serikali imetoa fedha nyinyi kutekeleza mradi huo na wao ndiyo wenye dhamana ya kuuendesha na kuusimamia mradi huo.

Kauli hiyo imetolewa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Augustine Vuma wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati hiyo ya kukagua chanzo cha umeme wa Gesi Asilia utakaotumika kuendesha treni hiyo ya kisasa katika eneo la kinyerezi, tarehe mkoani Dar es Salaam.

Vuma amesema TANESCO na TRC wahakikishe kuwa wanatunza na kulinda mradi huo kwa namna tofauti tofauti ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakuwa endelevu na kuleta tija ilikuyokusudiwa na kwamba Kamati haitegemei kusikia wala kuona miundombinu hiyo inaharibika kwa sababu ya uzembe.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wameshukuru kamati hiyo kufika katika eneo la mradi na kwamba wamepokea maelekezo yaliotolewa kuwa kutunza miundombinu kwa kuwa Serikali imetoa fedha nyingi sana kuwekeza katika miundombinu hiyo.

Amesema TANESCO watashirikiana na TRC kuhakikisha miundombinu hiyo inatunzwa na kutumia wataalamu wa ndani ambao wamepatiwa mafunzo maalum kutunza miundombinu hiyo kwa weledi mkubwa ili kuwanufaisha watanzania.

Pia amewataka Watanzania ambao wanaishi pembezoni mwa mradi huo kuendelea kulinda na kuitunza miundombinu hiyo kwa kuzingatia uzio uliowekwa na pia kupita maeneo mahsusi yalioruhusiwa kwa ajili ya usalama wao.

Katika mradi huo kumewekwa utaratibu mzuri wa kuwawezesha Wananchi kupita katika vivuko maalumu ili kuwaruhusu kuendelea na Maisha yao mengine ya kila siku.

Share: