Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea kituo Bandari Chongoleani cha Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP) na kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Kamati hiyo imetembelea Novemba 13, 2023 na kufanya ukaguzi wa mradi huo katika kituo kikuu cha kupokea na kuhifadhi mafuta ghafi Chongoleani, jijini Tanga.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. David Mathayo, ameongoza kamati katika ziara hiyo huku ikionesha kufurahishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa EACOP kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, jijini Tanga.
"Lengo la kamati ni kutembelea mradi huu na kujionea kasi ya ujenzi na kwa kweli tumefurahishwa sana na kasi ya ujenzi. Tulikuja mwaka jana tukajionea maendeleo, lakini leo tumekuta mambo tofauti kabisa, maendeleo ya ujenzi yamekua kwa kasi kubwa sana," amesema Mhe. Dkt. Mathayo.
Amewataka wananchi kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi huo, akiutaja utasaidia kuongeza Pato la Taifa pindi utakapokamilika Desemba 2025.
"Mradi huu ukikamilika utasaidia kuongeza Pato la Taifa na ajira, hivyo nitoe rai hasa kwa wakazi wa maeneo ambayo mradi huu unapita wachangamkie fursa zitokanazo na mradi ili waweze kuongeza kipato cha familia zao," alisema Mhe. Dkt. Mathayo.
Mwenyekiti huyo pia amesisitiza kuwa mradi huo ni muhimu utekeleze miradi ya kijamii katika maeneo yanayopitiwa na mradi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka amesema Wizara ya Nishati imepokea ushauri wa kamati na itasimamia vyema utekelezaji wake.
Amesema hadi kufikia tarehe 31 Oktoba 2023, serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilikuwa imetoa jumla ya Dola za Marekani 207 milioni kama mchango wake kwenye hisa ya kampuni ya EACOP, Watanzania 4,228 wameajiriwa na mradi, watoa huduma 146 wazawa walinufaika na kulipwa jumla ya Sh. 355 bilioni; wananchi 9,822 sawa na asilimia 99.2 wamelipwa fidia yenye jumla ya Sh. 35 bilioni. Hivyo, kazi inaendelea vizuri.