Kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti yaridhishwa na mradi wa umeme wa sgr

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeridhishwa na Utekelezaji wa Mradi wa njia ya Kusafirisha Umeme katika Reli ya kisasa (SGR).

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo ametoa pongezi za kamati wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati hiyo kwa lengo la kuona na kukagua utekelezaji wa njia ya kusafirisha umeme katika reli ya kisasa (SGR) iliyofanyika tarehe 11 Desemba 2023 mkoani Morogoro.

Sillo amesema wameridhishwa na utekeleza wa mradi huo baada ya kuona kazi iliyofanyika kwani kamati hiyo imekuwa ikitenga fedha za kutekeleza miradi mbalimbali nchini ukiwemo mradi huo.

Amewahimiza watekelezaji wa Mradi huo kukamilisha kwa wakati mambo machache yaliobaki ili mradi huo ukamilike kwa maslahi ya kukuza uchumi wa nchi na ulete tija kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameishukuru Kamati hiyo kwa kutenga muda na kukagua mradi huo ambao utachagiza shughuli za kiuchumi kwa Taifa.

Share: