Kamati ya bunge yasisitiza ushirikishwaji utekelezaji miradi

Haiwezekani tunajenga kituo kizuri cha afya mpaka kinakamilika wenzetu wa Tanesco wanakua hawajaleta umeme, maji yanakua hayajafika au barabara inakua haipitiki

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeshauri kuwepo kwa ushirikishwaji na uratibu baina ya miradi inayotekelezwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na taasisi zingine ili kuchangia kuleta maendeleo ya haraka kwa pamoja.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Denis Londo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya afya inayotekelezwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI katika Mkoa wa Lindi.

Mhe. Londo amesema ni vema kuwepo kwa ushirikishwaji wa taasisi zingine za miundombinu, maji na umeme kwenye miradi inayotekelezwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ili kurahisisha huduma kwa wananchi pindi inapokamilika.

" Ni vema kama tumepanga kujenga Zahanati au Kituo cha Afya basi tuwajulishe na wenzetu wa TARURA, Maji na Tanesco. Ili Kituo kinapokua kimekamilika basi kiwe na umeme, maji na barabara iwe inapitika."

"Haiwezekani tunajenga kituo kizuri cha afya mpaka kinakamilika wenzetu wa Tanesco wanakua hawajaleta umeme, maji yanakua hayajafika au barabara inakua haipitiki. Ni vema kukawa na cordination ya taasisi zetu kwenye utekelezaji wa miradi yetu hii," amesema Mhe. Londo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange ameiahidi kamati hiyo kuwa maelekezo yote yalitolewa yatafanyiwa kazi lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Kamati hiyo ya Bunge imetembelea miradi mitatu ya afya katika Wilaya mbili za Mkoa wa Lindi ambayo ni Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea, Kituo cha Afya Mtama pamoja na Zahanati ya Banduka na Mkwajuni.

Share: