Jkci yamshukuru rais samia kwa kuwapa magari

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia magari mawili ambayo yatatumika kutoa huduma za afya kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.

Shukurani hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Asha Izina wakati akizundua magari hayo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Asha ambaye pia ni mratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Rukwa aliongeza kuwa magari hayo yametolewa ili kusaidia katika huduma za afya ambapo katika Taasisi hiyo yatasaidia kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo watakaohitaji huduma ya gari la wagonjwa.

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya Wadhamini amesema Mhe. Dkt. Samia ametoa magari zaidi ya 700 katika Hospitali zote nchini kwaajili ya kutoa huduma katika hospitali ambapo JKCI imepokea magari mawili.

“JKCI tumepata magari mawili, moja likiwa gari la kuhudumia wagonjwa (Ambulance) na lingine kwaajili ya kusimamia usimamizi shirikishi unaofanywa na wataalamu wabobezi wa magonjwa ya moyo waliopo JKCI”, alisema Asha.

Asha amesema gari la kuhudumia wagonjwa litasaidia katika kazi za kuchukua wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Dar es Salaam pale litakapohitajika.

Share: