Ofisi ya Pensheni ya Hazina iliyo chini ya Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali inajukumu la kulipa mafao ya kustaafu kwa viongozi wa kitaifa na kisiasa na watumishi wa umma ambao hawachangii katika mfuko wowote wa hifadhi ya jamii.
Hayo yamebainishwa na Afisa Hesabu Mkuu kutoka Kitengo cha Pensheni Wizara ya Fedha, Bi. Joyce Chacky, wakati wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere Barabara ya Kilwa, Temeke, jijini Dar es Salaam.
Bi. Chacky alisema kuwa aina ya mafao ambayo hutolewa na Hazina kwa mstaafu ni pamoja na kiinua mgongo kwa mtumishi anapostaafu kwa mujibu wa Sheria akiwa na miaka 60 au akistaafu kwa hiari akiwa na miaka kuanzia 55.
Alisema aina nyingine ya mafao ni pensheni ya kila mwezi anayolipwa mstaafu baada ya kustaafu kwa mujibu wa Sheria Sura 371 ya mwaka 1956 na Sheria Na. 2 ya mwaka 2018 ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma.