Hasara kwa wanaohairisha safari za ndege

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameitaka Kampuni ya Ndege Air Tanzania (ATCL) kuja na mipango endelevu ya kumaliza tatizo la kuahirisha safari kwa ndege hizo mara kwa mara huku pia akitoa wito kwa Watanzania kutafuta mwarobaini wa kuahirisha safari kwa sababu inawanyima nafasi wengine wenye shida ya kusafiri ambapo amesema kwa August - October 2023 kituo cha Dar es salaam na Dodoma pekee kati ya Wasafiri 37,992 waliokata tiketi, Wasafiri 1,303 waliahirisha safari.

Akiongea na Menejimenti ya ATCL Jijini Dar es salaam, Kihenzile amesema “Wakati ananikabidhi taarifa Injinia Matindi nilimuuliza kwanini tiketi mara nyingi zinakuwa zimejaa lakini ukiingia kwenye ndege nafasi zipo, moja ya sababu nimeambiwa ni Watanzania tunakata tiketi halafu hatusafiri, ripoti inaonesha kati ya August, September na October mwaka huu abiria 37,992 walikata tiketi abiria 1303 hawakusafiri, fikiria walivyozuia nafasi za kusafiri achilia mbali hasara ya kipesa na hii ni kituo kimoja cha Dar - Dodoma”

Ameongeza kuwa “Hasara zake ni kwamba fedha ile haikuwa refunded kwahiyo ni hasara, kama ni Wafanyakazi wa kampuni zao kama ni Wafanyakazi Serikalini ni hasara kwa Serikali kama ni binafsi ni hasara kwenye Familia zao lakini pili wamezuia nafasi za Watu waliokuwa na shida muhimu zaidi ya kusafiri siku hizo.

Share: