Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba amewataka Maafisa Kilimo pamoja na Wakuu wa Idara ya Kilimo kuanzia ngazi ya Kijiji mpaka Mkoa kuhakikisha Wakulima wanajisajili ili kuweza kupata mbolea za ruzuku kwa wakati.
Mkuu wa mkoa Peter Serukamba ametoa maelekezo hayo Novemba 12,2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi yake wakati akizungumza na Wakuu wa idara ya kilimo, Maafisa kilimo , Mawakala wa mbolea, Kampuni za uzalishaji mbegu, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na Wakala wa udhibiti ubora wa mbegu (TOSCI).
"Wakulima wote wajiandikishe katika orodha ya watakaopata mbolea ya ruzuku na Maafisa ugani kazi yenu ni kuhakikisha mkulima anajiandaa vyema na msimu mpya wa kilimo kwa kuhakikisha wanapata mbegu bora, wanapanda mazao kwa usahihi na wanapata mavuno mengi na bora na kazi ya pili kwa Viongozi wa Serikali katika idara ya kilimo ni kuongea na wazalishaji na wauzaji wa mbolea ili kuhakikisha mbolea zinafika kila kata ili kufanikisha matumizi mazuri ya mbolea katika mazao tofautitofauti" amesema Serukamba.