Serikali ya Awamu ya Sita, imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wadau mbalimbali wanaohusika na mapambano dhidi ya UKIMWI nchini kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kuhakikisha kuwa wanatenga fedha za kutosha kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI nchini badala ya kutegemea wafadhili kwa kiasi kikubwa.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati wa Mkutano Maalum wa Wadau wanaoshughulikia Udhibiti wa UKIMWI Tanzania uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2023 mjini Morogoro na kuhusisha viongozi wa Serikali, Wadau wa Maendeleo na Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI.
Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Tanzania, kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI ambayo yamepelekea kupungua kwa maambukizi mapya, kupungua kwa idadi ya vifo vinavyotokana na UKIMWI, mwamko wa watu wanaotumia dawa (ARV) umeongezeka, maambuki ya Mama kwenda kwa mtoto yamepungua huku lengo likiwa ni kutokuwa na vifo vinavyotokana na UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Ameeleza kuwa, pamoja na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali pamoja na Wadau, bado UKIMWI haujadhibitiwa inavyotakiwa, hali inayoweza kupelekea maambukizi mapya kuongezeka hivyo ametaka wadau wote wanaohusika kuendelea na juhudi za utoaji afua mbalimbali zenye lengo la kumaliza UKIMWI.