Dkt. Nchemba azitaka taasisi za fedha za kimataifa kutoa mikopo yenye riba nafuu

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameshiriki mjadala ulioandaliwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ukiwashirikisha wawakilishi kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, unaofanyika Jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kuzitaka Taasisi za Fedha za Kimataifa kuzisaidia nchi zinazoendelea kwa kuweka mifumo rafiki ya kutoa mikopo yenye riba nafuu zaidi ili ziweze kutekeleza miradi na program mbalimbali zitakazochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Dkt. Nchemba alisema kuwa changamoto za mizozo ya kivita baina ya Urusi na Ukraine na maeneo mengine pamoja na UVIKO 19, vimesababisha nchi zinazoendelea kuyumba kiuchumi hivyo zinahitajika jitihada za makusudi kutoka Taasisi za Fedha za Kimataifa, ikiwemo IMF, kuingilia kati kunusuru mtanziko huo wa kiuchumi na kuziwezesha nchi hizo kuwahudumia wananchi wake kikamilifu.

Mjadala huo ulisimamiwa na Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa anayesimamia Kanda ya Afrika, Bw. Abebe Sellasie, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, Mwakilishi Mkazi wa IMF, Bw. Sebastian Acevedo na waalikwa mbalimbali kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, na umefanyika katika Hotel ya Sea Cliff, Jijini Dar es Salaam.

Share: