Katika Halfa hiyo Mhe. Dkt. Nchemba aliambatana na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb)
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewataka watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuongeza ubunifu, umahiri na kuhakikisha wanatenda haki wakati wa kukusanya mapato ya Serikali ili kutimiza matarajio ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuwaletea watanzania maendeleo ya uhakika.
Mhe. Dkt. Nchemba, amesema hayo wakati akihitimisha Kikao cha Tathmini ya Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC).
Mhe. Dkt. Nchemba ametumia fursa hiyo pia kuwapongeza TRA kwa utendaji kazi mahiri kwa mwaka wa fedha ulioisha wa 2023/24, ambapo walikusanya kiasi cha shilingi trilioni 27.64, ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 97.67 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 28.30, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 14.50, ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi trilioni 24.14 katika mwaka wa Fedha uliopita 2022/23.
Hata Hivyo amemwagiza Kamishna Mkuu Mpya wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, kuwachukulia hatua kali za kisheria na kinidhamu ikiwemo kuwafukuza kazi baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo wanaokiuka maadili ya kazi zao ikiwemo kudai na kupokea rushwa, kwa kuwa vitendo hivyo vinaitia doa Mamlaka na kuikosesha Serikali mapato.
Aidha amemwagiza Kamishna huyo kuwachukulia hatua kali wafanyabiashara wasiowasilisha ritani za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwa kuwa Fedha hizo zinatakiwa kuwasilishwa serikalini kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwani wafanyabiasharani Mawakala wa Serikali wa kukusanya kodi hiyo na hazitakiwa kufanywa kama ni sehemu ya mapato yao.
Katika Halfa hiyo Mhe. Dkt. Nchemba aliambatana na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), Kamishna Msaidizi wa Idara ya Sera Wizara ya Fedha, Bw. William Mhoja, na Maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha.