Dkt. Nchemba ametoa ombi hilo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko, Jijini Dodoma
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameiomba Indonesia kushirikiana na Tanzania kuboresha mifumo ya kodi ili kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuondoa changamoto zinazowakabili walipakodi nchini.
Dkt. Nchemba ametoa ombi hilo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko, Jijini Dodoma ambapo walijadiliana mambo muhimu ya kuimarisha ushiriakiano kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
Alisema kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto ya idadi ndogo ya walipa kodi pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya wafanyabiashara walioko katika sekta isiyo rasmi hivyo mfumo thabiti wa kodi unahitajika ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuongeza idadi ya walipakodi.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Indonesia ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa ya mifumo ya kodi na kwamba Tanzania itanufaika na ujuzi huo kwa kuwapa ujuzi zaidi maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Wizara ya Fedha kwa ujumla kujifunza Indonesia ilivyofanikiwa katika eneo hilo.
Aidha, Dkt. Nchemba aliishukuru Indonesia kwa mchango wake katika maendeleo ya nchi ambapo nchi hiyo imesaidia miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa ujuzi na utaalam kwa watanzania katika nyanja mbalimbali.
Katika mazungumzo yao, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Tatmiko, aliahidi kuwa nchi yake iko tayari kuendelea kuwapa ujuzi watanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo sekta za nishati, kilimo na biashara na kwamba iko tayari pia kuwajengea uwezo watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA namna ya kujenga na kutumia mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato.
Aidha aliahidi kuwa ataendelea kuhamasisha wafanyabishara kuja kuwekeza nchini ambapo amesema idadi kubwa ya wawekezaji kutoka nchini Indonesia wamekuwa wakiulizia mara kwa mara kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini, yakiwemo masuala ya utalii.